Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa idadi ya waliopata maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19) nchini imefika 284 na kwamba wagonjwa 11 wamepona, 256 wanaendelea vizuri na 10 wamefariki dunia.
Ameyasema hayo leo, Aprili 22, 2020 alipokuwa akiongoza maombi maalum ya kitaifa kukabiliana na virusi vya corona, yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Dar es Salaam na Zanzibar ndio maeneo ambayo maambukizi mengi yamebainika ukilinganisha na maeneo mengine nchini.
Ameeleza kuwa jumla ya watu 2,815 waliokuwa karibu na wagonjwa walifuatiliwa afya zao na kati yao 1,733 hawakuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Tanzania imejitahidi kupambana na maambukizi kwani hadi sasa iko chini ya kiwango kilichokuwa kimekadiriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa ifikapo mwishoni mwa Aprili, 2020 nchi yetu ingekuwa na wagonjwa 524,716 lakini tunashukuru Mungu kwakuwa kadirio hilo hatujalifikia,” amesema Waziri Mkuu.
Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, akiwasihi wasiokuwa na sababu za msingi wasitoke majumbani kwao.
Waziri Mkuu aliwataka pia wafanyabiashara kuona kama hawana sababu ya kwenda kwenye soko la Kariako wafanyie biashara zao katika maeneo waliyoko.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini kuendelea kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kupunguza misongamano kwenye nyumba za ibada na kupunguza muda wa kufanya ibada kadiri iwezekanavyo.
“Ninawaomba viongozi wa dini wachukue tahadhari zaidi kwa kuhakikisha mikusanyiko kwenye nyumba za ibada inapungua ikiwemo waumini kukaa kwa nafasi, umbali wa angalau mita moja kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na kuweka maeneo ya kunawa kwa maji ya sabuni pamoja na kutakasa mikono katika nyumba zote za ibada,” Waziri Mkuu amesema.
Idadi ya wagonjwa 284 ilifikiwa baada ya Wizara ya Afya kutangaza wagonjwa wapya 30, ikiwa ni zaidi katika idadi ya wagonjwa 254 waliokuwa wametangazwa awali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara, wagonjwa hao wapya wametoka katika mikoa ifuatayo ikiwa na idadi kwenye mabano; Dar es Salaam (10), Zanzibar (9), Mwanza (4), Pwani (2) na Dodoma (2).
Mikoa mingine iliyopata wagonjwa kati ya 30 wapya waliotangazwa ni Kagera, Manyara na Morogoro ambapo kila mkoa una mgonjwa mmoja.