Serikali imewataka wahandisi wote nchini kuendelea kujisajili chini ya Bodi ya usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) ili waweze kutambulika kitaifa na kimataifa .
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati akifunga maadhimisho ya 18 ya siku ya wahandisi nchini ambapo zaidi ya Wahandisi 3000 wamehudhuria huku Wahandisi 630 wakila kiapo.
Mhandisi Sanga amesema kuwa kujisajili kwa wahandisi ni takwa la kisheria hivyo mlango uko wazi kwa kila mhandisi kujisajili huku akihimiza kwa wahitimu fani ya uhandisi kutoka vyuo mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo.
“kufanya hivyo itasaidia zaidi wahandisi kuaminika kitaifa na kimataifa zaidi pamoja na kuepusha watu wanaofanya kazi ya uhandisi kutekeleza miradi ya miundombinu licha ya kuwa hawana vigezo hali ambayo husababisha miradi kutekelezwa kwa kiwango cha chini,” Amesema Mhandisi Sanga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wahandisi, Prof. Ninatubu Lema, amesema zaidi ya watu 800 wamefuatilia kwa njia ya mtandao hivyo idadi ya watu wote waliofuatilia ni zaidi ya 3700 ikivuka lengo ambapo matarajio ilikuwa ni watu 3200.
Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi Patric Barozi, amesema kuwa siku tatu kulihusishwa mijadala ya kitaaluma,Maonesho ya Ubunifu,Sayansi na Teknolojia huku pia Makampuni 61 yakishiriki.