Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limemtaka mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kueleza msimamo wake na kauli yake kuhusu tukio la kuvamiwa kwa mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika tukio hilo lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, watu hao wanaodaiwa kuwa na bastola na silaha za jadi walivamia mkutano huo na kuwapiga waandaaji pamoja na waandishi wa habari ambao wengine waliumia kutokana na purukushani za kutaka kujiokoa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini humo, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema kuwa kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif aliwaandikia barua akilaani kitendo hicho lakini hawakupata kauli na msimamo wa Profesa Lipumba licha ya kujaribu kuwasiliana naye.

Hata hivyo, Makunga alisema kuwa jukwaa hilo linatoa muda kwa Profesa Lipumba kuweka wazi msimamo wake kabla halijachukua hatua zaidi.

“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mikutano ya habari ya Profesa Lipumba na wafuasi wake. Hatujafikia hatua ya kuzuia kuripoti habari zake, tunampa nafasi kwanza, anaelewa msimamo wetu. Ikiwa hatutaridhika na hali ya usalama kwa waandishi wa habari tutalazimika kuchukua hatua zaidi,” alisema.

Aidha, Mwenyikiti huyo wa TEF aliliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kuhusika, huku akiwataka waandishi pia kuchukua tahadhari wanapokwenda kukusanya habari.

Siku mbili zilizopita, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya ambaye ni mfuasi wa kambi inayomuunga mkono Profesa Lipumba alikiri kuwa vijana waliovamia mkutano huo wanatoka katika kambi yao na kwamba walikuwa katika ‘doria’ ya kawaida.

Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Aprili 27, 2017
Chadema yakanusha kupokea barua ya bunge