Waajiri nchini, wameombwa kufuata sheria na kanuni mpya zilizowekwa na Serikali juu ya upandishwaji wa mishahara kwa wafanyakazi wote, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ndani ambao kima chao cha chini cha mshahara ni Shilingi 60,000 hali itakayowasaidia kumudu mahitaji muhimu.
Hayo yamesemwa na Viongiozi wa mtandao wa Wafanyakazi wa ndani Tanzania kutoka mikoa sita nchini, wakati wa semina wezeshi inayoendelea mkoani Mwanza.Mratibu kutoka shirika lisilo la kiserikali la Wote Sawa, Domitala Faustine akiishukuru Serikali kusikia kilio cha wafanyakazi hao.
Amesema, “pamoja na mambo mengine serikali imejitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi hawa lakini bado waajiri wameendelea kuwa wagumu hivyo tunaiomba serikali kuweka makazo juu ya kusisitiza juu ya swala hili wapandishiwe mishahara waweze kumudu mahitaji yao.”
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kufanya utaratibu wa kuanza kutekeleza mkataba wa kimataifa no 189 unaoeleza kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa ndani ili kuweza kukabiliana na matatizo wanayokutananayo wafanyakazi hao.