Wanafunzi wote waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu, wilayani Lushoto Mkoani Tanga wametakiwa kuhakikisha wanaripoti kwenye shule walizosoma na kuitwa majina kila Jumatano.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika ametoa agizo kwa wazazi wa wanafunzi wote waliohitimu kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti katika shule zao walizohitimu kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi hawatoki nje ya Wilaya au Mkoa wa Tanga hadi watakapochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.

Lugangika amesema ipo tabia ya baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto katika miji mikubwa ili kufanya kazi, jambo ambalo ni kinyume cha haki za watoto na wengi huwa hawaripoti shule hata wanapochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Aidha, Lugangika amewaagiza Walimu Wakuu na Maafisa Elimu kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa hadi wanafunzi watakapopangiwa Shule za Sekondari.

Wilaya ya Lushoto ina jumla ya shule za msingi 251, ambapo halmashauri ya Bumbuli ina shule 83 na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ina jumla ya shule 168.

Ndala: Tunakwenda Tanzania kuishangaza dunia
Bobi Wine asitisha kampeni

Comments

comments