Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewataka Watoa huduma za Afya nchini katika vituo vya binafsi na vya Serikali kutoa huduma kwa kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Dkt. Sichalwe amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa kujadili namna ya kuboresha utoaji huduma katika Sekta Binafsi ulioanza Aprili 12 Jijini Dodoma.
“Mazoea ya kutoa huduma yanaweza kupelekea mazingira magumu sana ya kutoa huduma bora ndio maana Serikali ikakubali Sekta binafsi ishiriki kwenye kutoa huduma lakini kwa utaratibu wa kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya.” Amesema Dkt. Sichalwe.
Sambamba na kufuata miongozo kwa usahihi, Dkt. Sichalwe ameelekeza upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba na vitendanishi vyenye ubora ikiwa ni sehemu ya vichocheo vya kutoa huduma bora kwa wananchi wanaoenda kupata huduma katika vituo.
Aidha, Dkt Sichalwe amesema huduma bora lazima ziendane na Watumishi wenye weledi wa kutosha, nidhamu, elimu na wanaofuata maadili ya taaluma yao kulingana na taratibu na Sheria za Mabaraza ya taaluma zao.
Kwa upande mwingine, Dkt. Sichalwe ameitaka Sekta binafsi kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa (survaillence) ili kutambua mapema magonjwa ya mlipuko na kuweka mikakati mizuri ya namna bora ya kupambana dhidi ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na Serikali.
Hata hivyo, Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa Sekta binafsi kuongeza ushirikiano kwa Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko pindi yanapoingia hali itayoongeza kasi katika kudhibiti maambukizi kwa wananchi.
Nae Mkurugenzi mkazi wa PharmAccess Dkt. Heri Marwa amesema, takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO zinonesha kwamba, udadi kubwa ya watu hufariki kwa kukosa huduma bora ukilinganisha idadi ya watu wanaoshindwa kwenda kupata huduma, hii inaonesha ni jinsi gani kama nchi tuna safari ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hata hivyo, Dkt. Marwa ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuwahudumia wananchi, hasa katika kipindi hiki ambacho kipaumbele cha Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kutoa huduma bora kwa wananchi.