Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema baadhi ya mashambulizi yanayotokea katika eneo la kusini mwa Tanzania mpakani na Msumbiji yanafanywa na vijana waliotoroka Tanzania baada ya kufanya vitendo kama hivyo katika mikoa ya Pwani na Tanga.
Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo katika Jeshi la Polisi Tanzania, Liberatus Sabas amesema kwamba baadhi ya vijana hao walitoroka shule na kujiunga na makundi hayo.
Amesema licha ya matukio hayo ya mashambulizi kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa, jamii ya Watanzania inatakiwa kufuatialia kwa karibu mienendo ya vijana katika jamii ili kukomesha hali ya vijana kujiunga na makundi ya uhalifu.
Sabas ameongeza kuwa polisi nchini imewakamata watu kadhaa kwa ushirikiano wa maafisa wa usalama wa Msumbiji, wakihusishwa na mashambulizi hayo.