Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema serikali itakuja na mpango wa namna ya matumizi ya mawe ya madini ya Tanzanite yaliyopatikana Mirerani, ambayo yameweka rekodi ya kuwa makubwa zaidi katika historia ya uchimbwaji wa madini.
Amesema kuwa madini hayo yamenunuliwa na serikali hivyo hata utaratibu wa kuyatumia utawekwa wazi hivi karibuni.
”Serikali itakuja na utaratibu wa namna gani mawe hayo yatatumika au kama ni kuwekwa kwenye makumbusho yetu bahati nzuri haya mawe yanamilikiwa na serikali hivyo utawekwa utaratibu na mtaelezwa hapo baadaye”, amesema Biteko
Aidha, amebainisha kuwa Pesa inayopatikana kupitia uchimbaji wa madini ya Tanzanite kwasasa inafikia mpaka Bilioni 50, hivyo mapato ya serikali nayo yamepanda kutoka Shilingi Milioni 70 hadi Bilioni 3.9 kwa mwaka.
”Ni mawe makubwa pekee ambayo yamepatikana kwa mara ya kwanza tangu historia ya kuchimbwa kwa Tanzanite, tukiangalia katika rekodi za serikali hakuna jiwe kubwa lenye kilo zaidi ya tano ambalo limewahi kupatikana” amesema waziri Biteko
Jana Juni 24, 2020, mchimbaji mdogo wa madini alitangazwa kuwa Bilionea mpya nchini, mara baada ya kuchimba na kuuza mawe mawili ya madini ya Tanzanite yenye jumla ya uzito wa Kilogramu 15 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.8.