Hospitali ya Meta jijini Mbeya imewekewa vyumba vinavyoruhusu wenza kuingia pamoja wakati wa kujifungua.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la mama na mtoto la hospitali ya Mbeya.
Amesema, ”Wakati wa kujifungua mwanamke anahitaji faraja, hivyo hospitali hii imeweka vyumba vya kujifungulia ambavyo vinaruhusu mwenza kuwepo. Hii itasaidia wanaume kujenga mapenzi juu ya wenza wao,”
Hospitali ya META itatoka kulaza wagonjwa 150 mpaka zaidi ya wagonjwa 300 kwa Kanda.
“Tutafuta fedha kwa wale kina mama wajawazito watakaoonekana wana matatizo mapema, wawekewe eneo la kufikia mpaka wakati wa kujifungua utakapofika,” ameongeza.
Pia Rais Samia ameahidi kuwa Serikali inaendelea kuweka huduma kadhaa za aina hii katika Kanda zingine pia nchi nzima kwani kwa kiasi kikubwa zinapunguza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua na vifo vya watoto.
Ujenzi wa jengo hilo umefikia zaidi ya 80%, na utakapokamilika Rais Samia atafika kwa ajili ya uzinduzi.