Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na wanasiasa wakongwe na wanazuoni wanaokiunga mkono chama hicho wanakutana kwa lengo la kukisuka upya ili kiwe imara zaidi.

Mkutano wa kufanikisha mkakati huo unafanyika katika hotel ya Protea – Aishi iliyopo Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Baadhi ya wanasiasa wakongwe wanaohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mzee Kingunge Ngombale Mwilu, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu mwenyekiti Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, manaibu katibu wakuu John Mnyika na Salum Mwalim.

Kikao hicho kinachodaiwa kuwakaribisha wataalam wa masuala ya kisiasa kutoka ndani na nje ya nchi kinatarajiwa kumalizika Januari 11 mwaka huu.

“Tunataka kuisuka upya Chadema baada ya uchaguzi huu uliomalizika, ambao ulitawaliwa na hila na ghiliba. Lengo letu, tunataka kujipanga kimkakati ili kukitoa chama chetu hapa kilipo na kukiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na hila za CCM na serikali yake,” Mmoja wa viongozi waandamizi ambaye hakutaka jina lake litajwe aliliambia gazeti la Mawio.

Imeezwa kuwa mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na baadhi ya wabunge wa chama hicho, umelenga katika kuyaleta pamoja makundi yote yaliyokuwa yanaunga mkono harakati za Chadema katika kuchukua dola.

Kikao hicho pia huenda kikatoka na majibu ya Katibu Mkuu wa Chama hicho atakayechukua nafasi ya Dk. Willbroad Slaa.

Azam FC Washindwa Kufikia Malengo Mapinduzi Cup
Saudi Arabia Yashambulia ubalozi wa Iran