Meneja wa Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke amefunguka kwa mara ya kwanza na kuweka wazi matarajio ya mchezaji wake kusalia Simba SC, baada ya mkataba wake wa mkopo utakapomalizika Msimbazi.
Baleke alisajiliwa Simba SC wakati Usajili wa Dirisha Dogo la usajili mwezi Januari 2023, kwa makubaliano ya mkataba wa miaka miwili akitokea TP Mazembe ya nchini kwao DR Congo.
Wakala wa Mshambuliaji huyo amesema Baleke ana mkataba miaka mitano na TP Mazembe na aliutumikia kwa miaka miwili akiwa kwao DR Congo, hivyo Simba SC ilichokifanya ni kununua Mkataba huo kwa miaka miwili, huku akiahidi kupambana kumbakisha Mshambuliaji huyo kwa mwaka mmoja zaidi Tanzania, ili kutimiza miaka mitano.
“Baleke alisaini mkataba wa miaka mitano na Tp Mazembe, hapo awali alishatumikia miaka miwili ikabakia mitatu, Simba SC wamemchukua kwa mkopo wa miaka miwili, hivyo akimalizana na Simba kule Tp Mazembe unasalia mwaka mmoja, sasa huo mwaka mmoja tutaifanyia kazi ili Baleke abakie Simba SC.” amesema
Amesema Baleke alilazimika kujiunga na Simba SC siku mbili kabla ya Dirisha la Usajili kufungwa mwezi Januari 2023, baada ya kushinikiza kuondoka kutokana na alikuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha TP Mazembe.
Hata hivyo Baleke alipelekwa kwa mkopo wa miezi Sita Nejmeh SC ya Beirut-Lebanon mwanzoni mwa msimu huu.