Wakala wa kiungo kutoka nchini Italia na klabu ya Chelsea Jorge Luiz Frello Filho (Jorginho), amesema huenda mteja wake akarejea kwenye ligi ya Serie A mwishoni mwa msimu huu.
Joao Santos wakala wa kiungo huyo mzaliwa wa Brazil, amesema lengo kubwa kupa nafasi mteja wake kuondoka London, England ni kutaka kumpa nafasi ya kufanya kazi kwa mara nyingine tena na bosi wake wa zamani Maurizio Sarri, ambaye kwa sasa anawatumikia mabingwa wa Italia Juventus FC.
“Inawezekana akaondoka, nitakaa chini ya mchezaji wangu ili kumsikiliza kama anahitaji kurejea Italia na kuachana na Chelsea.” Alisema wakala huyo.
“Nina matumaini makubwa atakua na furaha zaidi akicheza chini ya meneja Sarri, tofauti na sasa akiwa Chelsea, japo anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara.”
Jorginho alijiunga na Chelsea mwaka 2018, huku msikumo mkubwa wa kufanya hivyo ukitoka kwa meneja Sarri ambaye aliajiriwa Stamford Bridge akitokea SSC Napoli, iliyokua ikimiliki mchezaji huyo kwa wakati huo.
Alikua sehemu ya mafanikio Chelsea msimu wa 2018/19, na alifanikiwa kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha The Blues mara 37, huku akichagiza ushindi uliowapa ubingwa wa UEFA Europa League dhidi ya Arsenal mwaka 2019.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, ameendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Chelsea msimu huu chini ya meneja Frank Lampard, na tayari ameshafunga mabao manne kwenye michezo 23 aliyocheza.
Wakala Santos amesema njia atakayoitumia kufanikisha uhamisho wa mchezaji wake, ni kutumia mwanya wa kufikia kikomo mkataba wake wa miaka mitatu, ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu.