Wakala wa mshambuliaji kutoka nchini Hispania Lucas Perez amesema mchezaji wake yupo tayari kuachana na Arsenal iliyomsajili mwanzoni mwa msimu huu akitokea Deportivo La Coruña.
wakala wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 Rodrigo Fernández Lovelle, amesema sababu kubwa inayomsukuma Perez kutamani kuondoka jijini London, ni kuchoshwa na mpango wa kushindwa kucheza katika kikosi cha kwanza.
Amesema mchezaji wake ana uwezo wa kujumuishwa katika kikosi cha kwanza kila mwishoni mwa juma, lakini hali hiyo imekua tofauti tangu alipotua klabuni hapo, ambapo amecheza michezo miwili ya ligi kuu na kufunga mabao sita kwenye michuano yote.
“Ukweli ni kwamba, Lucas anataka kuondoka kwa sababu hana furaha tangu aliposajiliwa na Arsenal,” alisema wakala alipohojiwa na CalcioMercato.
“Amekua hana utulivu wa nafsi, na wakati mwingine hujihisi kama ametengwa na meneja wake Arsene Wenger, ambaye alitarajiwa kumtumia mara kwa mara kutokana na Arsenal kukabiliwa na tatizo la safu ya ushambuliaji.
“Haijalishi mustakabali wa meneja ama jambo lingine lolote, zaidi ya kutaka kuona mchezaji wangu anakua na furaha wakati wote, njia sahihi ni kuondoka na kusaka mahala pengine ambapo atapata nafasi ya kucheza kila mwishoni mwa juma.”
Perez alijiunga na Arsenal Agosti 27 mwaka 2016, kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 17.1.
Katika mchezo wa kombe la FA uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo, Pperez alifunga bao la kwanza kabla ya mshambuliaji mwenzake Theo Walcott hajaongeza la pili na kuiwezesha Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Sutton United.