Kampuni ya TNB Sports Agency Management inayomsimamia Ranga Chivaviro imemaliza tetesi za Mshambuliaji kuwatumikia mabingwa wa soka Tanzania Bara Young Africans msimu ujao 2023/24.
Chivaviro amekuwa akitajwa kuwa katika rada za Young Afrcans kabla ya msimu 2022/23 kumalizika, na hiyo ni kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika akiwa na MArumo Gallants na kufanikiwa kufunga mabo 06 nyuma ya Fiston Mayele aliyefunga mabao 07.
Mkurugenzi wa Kampuni ya TNB Sports Agency Management Herve Tra Bi amesema ni kweli walikuwa na mazungumzo na Rais wa Young Africans Hersi Said, kwa ajili ya kufanya biashara ya usajili wa Chivaviro, lakini kwa sasa mpango huo umekufa kufuatia Klabu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates kuweka fedha nyingi, kwa ajili ya uhamisho wa Mshambuliaji huo.
Kiongozi huyo amesema wanauheshimu Uongozi wa Young Africans kupitia Rais wake Hersi Said, lakini kwa mpango wa uhamisho wa mchezaji wao hawana budi kuwataka radhi kwa kusitisha mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea ili kufanikisha biashara kati yao na Kaizer Chiefs ama Orlando Pirates, ambazo zimedhamiria kukiwasha kisawasawa msimu ujao katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
“Tunamuheshimu Rais wa Young Africans, lakini kwa sasa hakuna uwezekano wa Ranga Chivaviro kutua katika klabu hiyo ya Tanzania, awali tulikuwa na mazungumzo ambayo yalikwenda vizuri sana lakini mambo yamebadilika.”
“Mchezaji alikuwa ameshakubali kucheza soka Tanzania, lakini ofa zilizowasilishwa kwetu zimebadili kila kitu na sasa kuna uwezekano wa Chivaviro kubaki Afrika Kusini.”
“Klabu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates zimeleta ofa bora zaidi, na sisi TNB Sports Agency Management tumeona tufanye biashara nzuri kwa maslahi ya mchezaji wetu.” Amesema Mkurugenzi Herve Tra Bi