Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi 6 ya maji kati ya RUWASA na Wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo, yenye thamani ya Shilingi Bilioni 9.68 itakayonufaisha watu zaidi ya 83,000 katika Wilaya tano.
Akizungumza hii leo Novemba 20, 2023 kabla ya utiaji saini wa mikataba hiyo, Sendiga aliwataka wakandarasi hao kutekeleza majukumu yao sawa na mkataba unavyoelekeza na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada (Extension), utakaoongezwa kwenye utekelezaji wa mikataba hiyo.
Aidha, Sendiga amezipongeza Mamlaka za Maji Manyara RUWASA na Babati BAWASA, kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kutoa huduma za maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara.
Mapema hivi karibuni, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema matokeo ya Tathimini ya Hali ya Upatikanaji wa Maji Vijijini katika Vijiji 12,314, iliyofanywa na Wizara ya Maji na kupelekea kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini-RUWASA, Wizara imefanikiwa kupeleka maji katika vijiji 9,671 na vijiji 2,643 vilivyobaki vitakamilika ndani ya miaka miwili ijayo.