Wakazi wa jiji la Mbeya wameiomba serikali kupunguza gharama za kuhifadhi na kuosha maiti katika mochwari ya hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya.
Wamesema kuwa kwa sasa fedha wanazotozwa kwa ajili ya kuwaandaa ndugu zao walio poteza maisha ni kubwa na hailingani na hali ya uchumi wa maisha yalivyo sasa.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila wakati wa usikilizaji wa kero kwa wananchi wa Kata ya Sinde Mkoani humo wamesema kuwa wamekuwa wakitozwa sh. 50,000 kwa siku kwa ajili ya kuhifadhi mwili na sh. 20,000 kwa ajili ya kuosha maiti katika hospitali ya rufaa ya kanda.
Aidha, wameongeza kuwa wahudumu wa hospitali hiyo wanapo ona mgonjwa amezidiwa mahututi na hawezi kupona huwaeleza ndugu kununua dawa za gharama kubwa na kwamba inapotokea mgonjwa kafariki wahudumu hao huzichukua dawa na kuziuza.
Akijibu malalamiko hayo, mkuu wa mkoa wa mbeya, Albert chalamila ameahidi kuwasiliana na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto ili kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo, kwani hospitali hiyo ipo chini ya wizara, hivyo yeye hana mamlaka ya moja kwa moja kutatua tatizo hilo, lakini atafuatilia bega kwa bega kupata ufumbuzi.