Waziri Mkuu Kassim Majalwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha wanaotaka kuhama kwa hiari yao wajitokeze na waseme wanataka kwenda wapi.
Majaliwa ametoa kauli hiyo Alhamisi, februari 17, 2022, wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani Ngorongoro.
Amesema kuwa Ngorongoro kuna idadi kubwa ya watu na kulishakuwa na mapendekezo hapo kabla lakini hapakuwa na ufanikishaji wa mpango huo.
“Suala la idadi ya watu ni kubwa. Kumbe huko nyuma kulishakuwa na mapendekezo. Yeyote anayeona anaweza kuishi mahali pengine yuko huru kusema. Kama yuko mtu wa aina hiyo, awe huru kwenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) kajiandikishe na Serikali itakuhudumia vizuri,” alisema
“Hayo ni maamuzi ya mtu binafsi, kusiwe na mtu wa kumshinikiza fulani asifanye maamuzi yake. Kama yuko aachwe afanye maamuzi yake, aseme anataka kwenda wapi na sisi tutamhudumia.” Amesema Majaliwa.
Hivi karibuni kuliibuka mjadala Bungeni kuwa Wakazi wa Ngorongoro wamekuwa wengi na mifugo mingi hali inayowanyima uhuru wananchi hao.