Wakenya wanaotumia mitandao ya kijamii wako katika hatari ya kukutana na kifungo cha miaka mitano jela au faini ya shilingi milioni 22 za Tanzania ($10,000) kwa kutumia lugha isiyo na staha kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu nchini humo.
Kwa mujibu wa Nairobi News, hali hiyo imetokana na pendekezo lililotolewa kwa lengo la kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Pendekezo hilo ni sehemu ya kanuni zinazoandikwa kwa ushirikiano wa vyombo viwili vya serikali ambavyo ni Mamlaka ya Mawasiliano na Tume ya Utaifa na Ushirikiano nchini humo.
- Wanaopost picha za watoto wao Facebook, Instagram kushtakiwa
- Sehemu ya pendekezo hilo inasema, “maudhui yote ya mitandao ya kijamii yataandikwa kwa lugha ya kistaarabu ambayo inaepuka maneno ambayo yanaleta chuki, ukabila na uchochezi.”
Imeeleza kuwa maudhui yote kwenye Facebook, Twitter na WhatsApp itakuwa ikifuatiliwa na yatakapobainika kuwa hayana ukweli na yametengenezwa kwa lengo baya, waliohusika kuyaandaa watakumbwa na mkono wa sheria.
Wakenya wanatarajia kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Agosti 8 mwaka huu. Umoja wa vyama vya upinzani vya NASA ambavyo vinamnadi Raila Odinga kama mgombea urais, na umoja ulioundwa na chama tawala JUBILEE wakimnadi Rais Uhuru Kenyatta wanaendelea na kampeni.