Wapiganiaji Uhuru Nchini Kenya, wamepaza sauti kumtaka Mfalme Charles III wa Uingereza na mkewe, Malkia Camilla ambao wameanza ziara yao ya Kiserikali ya siku nne nchini Kenya kuomba radhi kwa mateso waliyoyapitia.
Mfalme Charles anakabiliwa na miito ya kumtaka aombe radhi kutokana na historia ya umwagaji damu uliosababishwa na ukoloni wa nchi yake, wakati wakipigania uhuru wa Taifa hilo linalojiandaa kuadhimisha miaka 60 ya uhuru Desemba, 2023.
Ziara hiyo, ni ya kwanza ya Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 tangu alipovishwa taji la ufalme Septemba 2022 baada ya kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II.
Mfalme Charles na mkewe, Camilla, walikaribishwa katika hafla rasmi na Rais wa Kenya William Ruto Ikulu ya Nairobi ambapo mwenyeji wao huyo aliisifu ziara hiyo akisema ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.