Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi, amesema alifanya jitihada za hali na mali katika kuwapatanisha Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto lakini jitihada zake ziligonga mwamba.
Wakati wa mazishi ya mamake kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto siku ya Jumatano, Juni 22, Kericho, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alieleza juhudi zake za kusuluhisha suala hilo kati ya viongozi hao wawili.
Muturi alifichua kwamba aliwahi kuunda kikosi cha makasisi ili kuzima uhasama kati ya wawili hao, lakini haikufaulu.
Muturi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwaambia Wakenya sababu zilizomfanya ashindwe kuridhiana na naibu wake William Ruto akisema kwamba amekuwa akitafuta mara kwa mara majibu kutoka kwa Uhuru kuhusu suala hilo bila mafanikio.
Muturi, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa kiongozi wa taifa alisema kwamba juhudi zake ni pamoja na majaribio ya kumtaka Kadinali mstaafu John Njue kuwapatanisha wawili hao.
“Mnamo Januari 2020, nilijitwika mzigo wa kumtafuta aliyekuwa Kadinali John Njue kuunda timu ndogo ya makasisi wakuu ili kwenda kumuuliza Rais Kenyatta sababu za mfaragano huo na kutaka kuwapatanisha. Lakini hawakufaulu,” Muturi alifichua.
Spika aliongeza kuwa Wakenya wanastahili maelezo yenye kusadikisha yaliyojiri kati ya viongozi hao wawili waliokuwa kama kaka wa toka nitoke katika muhula wao wa kwanza uongozini.
Alisema majibu haya yanaweza kutolewa na Uhuru pekee na wala si porojo kwenye majukwaa mbalimbali.
“Wakenya wanastahili kuambiwa kilichoharibika kati ya Rais Kenyatta na Naibu wake. Rais anapaswa kujitokeza na kusafisha hewa kabla ya kuondoka madarakani mwishoni mwa muhula wake. Maelezo hayo hayawezi kutoka kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa Rais,” aliongeza Muturi.
Muturi alisema kuwa Uhuru alitengwa baada ya kupoteza washirika wake wakuu katika muhula wake wa pili na wa mwisho uongozini.
Uhusiano baridi baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto umejadiliwa zaidi kipindi hicvi cha kampeni nchini Kenya hususan katika ulingo wa kisiasa.