Mwenendo wa kesi inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inayoendelea kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imechukua sura mpya baada ya Wakili aliyekuwa anawatetea vigogo hao kujiondoa.
Wakili huyo anayefahamika kwa jina la Jeremiah Mtobesya amechukua uamuzi huo leo Mahakamani hapo baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali ombi waliloliwasilisha la kutaka kesi hiyo kuahirishwa ili kusubiri maamuzi ya rufaa iliyofunguliwa katika Mahakama ya Rufani.
Uamuzi huo wa wakili Mtobesya umefikiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbert Mashauri.
Viongo wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwa ni pamoja na kufanya mkusanyiko usio halali na kuhamasisha maandamano kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni.
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ilichukua uamuzi wa kutupilia mbali ombi lililowasilishwa na wakili wa viongozi hao wa chadema kwakuwa kifungu cha sheria walichotumia cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 hakiipi Mahakama hiyo mamlaka hayo.