Inaelezwa kuwa bado kuna sintofahamu kati ya Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans na Wachezaji kutoka DR Congo ambao wanadaiwa kutaka kuboreshewa maslahi yao kabla ya msimu wa 2023/24 haujaanza.
Wakongomani hao ambao wapo katika mtifuano na Uongozi wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni Joyce Lomalisa Mutambala, Yannick Bangala Litombo, Fiston Kalala Mayele, Jesus Moloko na Djuma Shaaban.
Kwa mujibu wa habari kkutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa wachezaji hao wanahitaji kuongezewa mishahara kutokana na kazi kubwa ambayo wameifanya katika msimu uliomalizika hivi karibuni.
Habari hizo zilieleza kuwa, Wakongomani hao hata msimu wa 2021/2022 ulipomalizika waliomba kuboreshewa mikataba jambo ambalo viongozi walilikamilisha kwa wakati.
“Sasa hivi viongozi wanaendelea kupambana kuzungumza nao waweze kuelewana kabla ya msimu mpya haujaanza, wote bado wana mikataba hivyo mazungumzo yanaendelea,” amesema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwani yeye siyo msemaji wa klabu.
Akizungumzia hilo, Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema uongozi unaendelea kufanya tathimini ya msimu uliopita na kujua wapi wanatakiwa kufanya marekebisho.
Amesema kama kuna mchezaji au mfanyakazi mwingine yoyote watakuwa wanataka kuachana nae au kuboresha maslahi yake, watakubaliana kwa utaratibu na kumaliza jambo hilo salama.
“Tupo katika mazungumzo na wale ambao mikataba yao inafikia ukingoni, pia tunazungumza na wale ambao hatutakuwa nao, ili kumaliza suala lao kwa amani,” aamesema afisa huyo.
Hadi sasa Young Africans imetangaza kuachana na wachezaji wanne ambao ni Benard Morrison, Tuisila Kisinda, Abdallah Shaib ‘Ninja’ na Dickson Ambundo.
Msimu uliomalizika hivi karibuni, Young Africans iliweka rekodi ya kutwaa mataji matatu kwa mara ya pili mfululizo ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA wakati wakifika hatua ya Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAFCC’.