Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali inatarajia kuweka luninga kwenye Minada itakayoonesha bei elekezi zitakazotumika katika uuzaji na ununuzi wa mazao.
Bashe ameyasema hayo hii leo Juni 8, 2022 wakati akiongea na wananchi wa Biharamulo na kusema Wizara yake imekusudia kutatua kero za wakulima na kusimamia miradi mbalimbali ya uzalishaji wa mazao.
“Mbali na uuzaji wa mazao wa bei elekezi za Tv za minadani hapa Biharauro tumegawa kilo 15,000 za mbegu ya alizeti na tunatarajia kuleta mbegu nyingine za zao hili hili zitagawiwa bure ili wakulima waweze kuzalisha zaidi,” aliongeza Bashe.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya Muleba iliyopo Mkoani Kagera, Toba Nguvila amewataka wenye uhakika na uwepo wa kikosi kazi kinachoendesha doria ya kukamata na kuwanyang’anya mazao wakulima kutoa taarifa ili zichukuliwe hatua stahiki.
Nguvila ameyasema hayo hii leo Juni 8, 2022 Wilayani Muleba kufuatia kauli ya Mbunge wa Muleba Kusini, Oscar Kikoyo kudai kipo kikosi kazi kinachafanya matukio hayo kwa wakulima wanaotoka kuvuna mazao yao.
“Hakuna mtu aliyechukuliwa mali yake na ikataifishwa na upo utaratibu wa usimamizi wa zao hilo na ndio tunao utekeleza kila siku kama kuna mwenye uhakika kwamba kuna matukio hayo ajitokeze tuchukue hatua,” alisema Nguvila.
Hata hivyo alikiri kuwepo kikosi kinachoundwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo na kukanusha tuhuma za kukamata, kunyang’anya na kupiga faini wakulima wanaosafirisha kahawa kutoka shambani.
Mbele ya Rais Samia na Wananchi wa Wilaya ya Muleba, Mbunge Kikoyo alitoa malalamiko akidai vitendo vya uporaji wa mazao ya wakulima vinaashiria uchonganishi kati ya Wananchi na Serikali yao.
“Bashe aliwahi kukemea vitendo hivi lakini tatizo linatatuliwa linarudi si sawa mkulima atoke shambani halafu akamatwe, akienda kukoboa pia anakamatwa na kutozwa faini mbona wakati analima hakamatwi,” alihoji Kikoyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ya siku tatu iliyoanza leo Juni 8, 2022.