Serikali imetangaza dhamira yake ya kuwalipa wakulima 156 wa mahindi jumla ya Shilingi milioni mia tatu kutokana na kuzulumiwa na mwenyekiti wa Chama cha Ushirika, Linus Kalandamwazye.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.

Malipo hayo yatawahusu wakulima wa Tarafa ya Mwimbi yenye kata nne ambazo ni Mambwe Kenya, Ulumi, Mkombo na Mwazye kutokana na kupima mahindi yao zaidi ya Tani 622.679 kwenye Chama cha Muzia Amcos kilichopewa uwakala na serikali wa kununua mazao kwa wakulima tarehe 8 Agosti 2017 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya wiki tatu lakini hawajalipwa mpaka sasa.

“Kesi ikiwa mahakamani serikali haiwezi kuingilia badala yake wakati tunaendelea na kesi hiyo ninaziagiza taasisi zangu tatu kuchanga fedha kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao” alisema Hasunga

Amesema wanaotakiwa kuchanga fedha hizo kwanza ni Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kulishughulikia jambo hilo kwa wakati ili wakulima hao waweze kulipwa fedha zao.

Ameiagiza pia tume ya Maendeleo ya Ushirika kuchanga fedha hizo kwani wao ndiyo wasimamizi wa Vyama vya Ushirika lakini kwa kipindi chote wameshindwa kushughulikia changamoto hiyo ya wakulima.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli haina dhamira ya kuwadunisha na kuwafedhehesha wananchi badala yake imejipambanua kuwanufaisha wakulima katika kilimo.

Alisema kuwa serikali imeamua kuwalipa fedha hizo wakulima ili kuendelea na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo lakini kesi itakapomalizika serikali itazidai fedha hizo.

Hasunga amemuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Rukwa kupanga vizuri madai ya wakulima hao huku akisisitiza kutoingizwa majina mapya (Majina Hewa) yasiyohusika na madai ya fedha hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amempongeza Hasunga, kwa kukubali kulivalia njuga jambo hilo kwa kuwalipa fedha hizo wakulima kwani kufanya hivyo kutarahisisha wakulima hao kuendelea na uzalishaji wa mazao katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.

 

Cristiano Ronaldo atinga anga za magwiji wa soka duniani
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 15, 2019