Kuwekeza katika kilimo cha Umwagiliaji kunaweza kuwa ni njia sahihi ya kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kuleta athari kubwa.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba alipokuwa akifunga kongamano la Wakulima lililoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Amesema kuwa Serikali imeweza kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya Umwagiliaji na kuchukua jukumu kubwa la kutoa mafunzo ya matunzo ya miundombinu hiyo kwa wakulima, ili kuweza kukabiliana na athari na hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
“Ili kuweza kufikia lengo hili ni lazima serikali na wakulima kwenda pamoja ili kufanikisha, hali ambayo inaweza pia kusaidia wakulima nao kuingia zaidi katika kilimo cha biashara kama vile wakulima wa skimu ya Lemkuna na Pawaga, pamoja na kuwa na uhakika wa chakula nchini.” Amesema Mhandisi Mbogo.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Marco Ndonde amesema kuwa Tume hiyo imejipanga kuboresha Miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya kilimo na mashirika mbalimbali ya maendeleo.
”Sambamba na hilo Tume ina mpango wa kujenga mabwawa ili kufanya kilimo cha umwagiliaji kiwe na uhakika wa kupata maji ya kutosha pamoja na kufungua miradi ya kilimo hicho kitakachoajiri vijana kutoka vyuo vikuu nchini.”amesema Ndonde
Akiwasilisha mada katika siku ya mwisho ya kongamano lililoshindanisha vyama vya wakulima wa umwagiliaji nchini, Fundi Mihayo kiongozi wa skimu ya umwagiliaji ya Mkombilenga iliyopo Mkoani Iringa amesema kuwa lengo la Serikali kuwezesha wakulima kuuza mchele badala ya kuuza mpunga katika maeneo ya skimu za kilimo cha umwagiliaji limefanikiwa kwa kisia kikubwa kwani kwa sasa skimu nyingi zimeweza kufunga mashine za kukoboa nafaka kama vile mpunga, na kupaki katika madaraja na ujazo tofauti.
Skimu ya umwagilijai ya Mkombilenga iliyopo katika kanda ya Mbeya imeibuka kidedea ikifuatiwa na skimu ya Lemkuna ya kanda ya Dodoma na skimu ya Nyida iliyopo katika kanda ya Mwanza kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.
Kongamano hilo la siku mbili lilishirikisha wakulima, wataalam wa kilimo toka ngazi za Mikoa, Wilaya, Kanda za Umwagiliaji, Tamisemi na Ofisi za Tume ya Umwagiliaji.