Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imelenga kurejesha zao la shayiri na kutatua changamoto zilizopo katika sekta ndogo ya Zabibu ili kuweza kukuza soko la mazao hayo na kuinua kipato cha wakulima wake.
Amebainisha hayo leo June 10 katika Mkutano uliyohudhuriwa na wanunuzi wa zao la zabibu na shayiri pamoja na wakulima wa mazao hayo.
Aidha Bashe amesema kuwa kwa sasa wakulima wa shayiri hawana soko, hivyo ni vyema kwa msimu ujao wakulima walime zao la shayiri na kupata soko.
“Lengo ni kutaka wakulima waweze kulima kwa msimu ujao na sisi serikali tutahakikisha mikataba inakuwa sawa kwa pande zote mbili kwa mnunuzi na mkulima na uwazi wa mikataba hiyo ili kila mmoja kunufahika katika zao hilo”, ameeleza Bashe.
Hata hivyo katika mkutano huo amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa na warajis wa vyama vya ushirika watakapo saini mikataba hiyo na Serikali ishirikishwe kikamilifu ili kulinda maslahi ya mkulima na wanunuzi.
Kwa zao la zabibu amesema msimu wa kilimo unaanza mwezi wa nane hivyo Serikali inahitaji uhakika wa masoko na wanunuzi wanatakiwa kusema namna ambavyo watanunua zao la zabibu .
“Hatutaki wakulima wa zabibu mwezi wa nane wakati wa kuvuna wapate shida ya masoko na nahitaji kujua kwa mwezi huo tutavuna kiasi gani .
Mkurugenzi wa Tanzania Bruweries (TBL) Philip Redman amesema kwa msimu ujao wa 2021, wameingia mkataba na wakulima 300 na kiwanda kina uwezo wa kuchukua tani 5,000 kwa mwaka.
Kwa upande wa Serengeti Breweries (SBL) Mkurugenzi wa Mahusiano Bw.John Wanyancha amesema kuwa kwa msimu ujao wanatarajia kuchukua tani 3,000 kwa wakulima 60.