Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewataka Wakulima na wafugaji kuendeleza utunzaji wa mazingira, na kwamba Serikali imejipambanua katika uwekezaji kwenye kilimo na mifugo ili sekta hizo mbili ziwe na manufaa.

Jafo amesema hayo alipotembelea mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro, na kudai kuwa endapo mazingira yataharibiwa, sekta za kilimo na ufugaji zitaathirika na ukame uliosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Amesema, “tunapokata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadanu kwenye vyanzo vya maji tunasababisha mito yetu kukauka na mito ikikauka kilimo chetu kinachotegemea mvua hakitakuwa na tija, nawaomba tutunze mazingira,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Jafo aliwapongeza waandaaji wa maonesho hayo yanayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani maandalizi mazuri ambayo yanatumika kutoa elimu kwa makundi hayo na wananchi kwa ujumla, na kuwataka Watanzania kuungana kulinda rasilimali zilizopo hapa nchini.

DPA, Taasisi Elimu ya juu wajielekeza tafiti ukatili wa kijinsia
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 7, 2023