Wakulima, katika skimu ndogo ya kilimo cha mbogamboga ya Iganjo iliyopo Uyole nje kidogo ya jiji la Mbeya, wameomba wataalam kutoka wakala wa vipimo kuwatembelea ilikuweza kusaidia tatizo la vipimo halisi vya mazao yao ambavyo vinafanywa katika hali ya udanganyifu na kuwasababishia hasara.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama cha Wamwagiliaji Iganjo. John Soda alipokuwa akizungumza katika eneo hilo ambapo amesema kuwa suala la kuzidisha ujazo unaotakiwa (lumbesa) bado ni tatizo jambo ambalo linawasababishia wao kama wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya hasara.
Soda amesema kuwa kumekuwa na tatizo la upimaji wa mazao katika magunia ambapo magunia yanayokaguliwa yanakuwa na vipimo halisi lakini magunia yanayokwenda sokoni yanakuwa hayana uhalisia.
“Tunawaomba wakala wa vipimo waweze kuja kututembelea na kusimamia kwa ukaribu suala hili la udanganyifu katika vipimo, jambo ambalo kwa kiasi fulani limekuwa likitusababishia hasara sisi wakulima wa mbogamboga hasa katika zao la viazi, vitunguu na Karoti, Pamoja na hilo naiomba serikali iweke utaratibu wa kuuza mazao nakutoa bei elekezi.” amesema Soda.
-
Safari za Zanzibar, Dar zasitishwa
-
Video: NECTA yatangaza matokeo ya Darasa la Saba
-
Wakulima wagoma kuuza korosho mbele ya Waziri wa kilimo
Kwa Upande wake, Solomon Soda Mkulima katika skimu hiyo aliishukuru Serikali kwa ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika skimu hiyo na kuiomba iendelee kuwasaidia waweze kupata pembejeo kwa bei ya ruzuku, nakumalizia kuboresha miundombinu katika sehemu iliyobakia.
Hata hivyo, kwa upande mwingine wakulima hao wameeleza kuwa kilimo cha umwagiliaji kimewanufaisha pakubwa.