Taasisi ya utafiti wa kilimo Tari-Ukiriguru wametengeneza zana ambayo ni mahususi kwa kupandia mbegu za pamba na inachukua muda mfupi kupanda shamba kubwa.
Dauson Malela mtafiti na mbunifu kutoka TARI-Ukiriguru amesema hayo jijini Dodoma katika viwanja vya Jamhuri katika maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu ya mwaka 2022 yanayoendelea.
Malela amesema zana hiyo ina uwezo wa kupanda kwa sentimita mia moja sitini kutoka mstari hadi mstari na sentimita thelathini mstari hadi mstari kitu ambacho awali haikuwezekana.
“Niseme tu Zana hii ni mahususi kwajili ya kutatua Changamoto zinazomkumba mkulima, inatumia saa moja na nusu hadi masaa matatu kupanda eneo lenye ukubwa wa hekari moja, Tofauti na hapo Mwanzo mkulima alikuwa anaweza kutumia masaa kumi na moja kupanda eneo lenye ukubwa wa hekari moja kitendo ambacho kinamfanya mkulima kutumia muda mwingi shambani akiwa ameinama na kinapelekea maumivu ya mgongo na kushindwa kuvumilia na kuamua kupanda eneo dogo huku badae akipata mazao kidogo,” amesema Malela.
Ameongeza “sisi kama wabunifu tumeliona hilo ndiyo maana leo tumekuja na mwarobaini wa Zana hii kwajili ya kuboresha mavuno kuokoa muda na mkulima kuweza kupata mazao mengi kwa wakati mmoja na kuongeza kipato cha mkulima mdogo,”
Sambamba na hilo amesema tafiti zinaonesha kwamba kila mkulima ambaye atatumia mashine hiyo kupanda mbegu kwenye eneo la heka moja ana uwezo wa kupata mazao kilo elfu moja na Mia tano.
Amesema awali wakulima walikuwa wanapanda mazao kwenye eneo lenye ukubwa wa heka moja kwa nafasi ya sentimeta tisini kutoka mstari hadi mstari na sentimita arobaini kutoka mmea hadi mmea hali iliyokuwa inapelekea mkulima kupata mavuno kidogo.
“Mashine hii inakokotwa na ng’ombe au kuvutwa na mtu ikiwa inaendelea kutembea inadondosha mbegu, hivyo wakulima kwa kutumia mashine hii itawasaidia kuokoa muda wakukaa shambani pia itainua kipato Cha mkulima mdogo.” amesema.
Aidha alisema utafiti umeonesha mashine hii inauwezo wa kupanda mbegu aina mbalimbali, kama alizeti kwa ukubwa tofauti sambamba na mahindi.
Kwa upande wake Robert Alphonce mtafiti na mbunifu kutoka taasisi ya kilimo Tari-Ukiriguru ametoa wito kwa Serikali iwasaidie Fedha ambazo zitawasaidia kuboresha vifaa vya kutengenezea mashine hizo kwa wingi kuongeza karakana hizi kwa wingi .