Serikali Nchini, imeanza kupanua wigo wa Kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga Shilingi 900 Bilioni huku ikisajili wakulima katika mfumo wa kidigitali ili kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba pamoja na aina ya mazao wanayolima.
Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo – FAO, Dkt. Dongyu Rome, Italia nje ya Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani na kuongeza kuwa usajili huo unalenga kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani kwa wakati zikiwemo pembejeo.
Amesema, “Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu/ Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula. Pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini.”
Majaliwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na kuhakikisha kinasimamiwa kwa kiwango cha juu ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kuuza nje na kudai kuwa usajili huo hautaishia kwa wakulima pekee bali utawahusu na Wavuvi, Wafugaji na watumiaji wa ardhi.