Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kutoa mikopo ya moja kwa moja yenye thamani ya shilingi 78.54 Bilioni kwa wakulima 119,797 wanaojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi, huku uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kwa asilimia 4.3 kutoka tani 769,966.66 mwaka 2021/2022 hadi tani 803,264.32 mwaka 2022/2023.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo jijini Dodoma na kuongeza kuwa, kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo pia imetoa dhamana ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 12.95 na kunufaisha wananchi 961 katika mikoa 20 katika shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi.
Amesema, “katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuongeza uzalishaji na tija; kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, na upatikanaji wa pembejeo. Vilevile, itaendelea kuimarisha huduma za ugani na upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo na kuwajengea uwezo wakulima wadogo.
Kuhusu kuimarika kwa huduma za ugani ikiwemo utoaji elimu kwa umma juu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa wa kibiashara Waziri Mkuu amesema umesababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa kufikia lita bilioni 3.62 katika mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na lita bilioni 3.4 mwaka 2021/2022.