Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wametakiwa kutenga fedha katika mipango ya bajeti za halmashauri zao ili kununua dawa ya kupulizia wadudu wanaosababisha maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wanaohusika kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.

Amesema endapo watafanikisha ununuaji wa dawa hizo na kuzifanyia kazi kiufasaha watakuwa wanafanikisha mkakati wa Tanzania wa kutokomeza ugonjwa huo nchini kutoka maambukizo ya asilimia 7.3 kwasasa hadi asilimia moja ifikapo mwaka 2030.

“Sitarajii kuona katika bajeti zijazo halmashauri hazitengi fedha kwa ajili ya kudhibiti na kutokomeza mazalia ya mbu bajeti hizo hazitapita maana lengo la kutenga fedha hizo ni kufanikisha mpango wa kuzuia na kutokomeza ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine,” amesema Gwajima.

Aidha amefafanua kuwa wataalamu wa halmashauri wanajua ni maeneo gani yenye mazalia mengi ya mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria ili wafanye tahmini halisi ya dawa inayohitajika na kuagizwa katika kiwanda cha kibaha kinachozalisha dawa zinazotumika kupulizia kwenye mazalia na kudhibiti ongezeko la wadudu.

“Wakurugenzi hawa walichukua hizi dawa kibaha hawajalipa, sasa ni lazima kwanza walipe deni, kisha wapange kwenye bajeti zao kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa kuwashirikisha wataalamu wa halmashauri ambao watatoa maelekezo juu ya kiasi cha dawa kinachohitajika,” ameongeza Naibu Katibu huyo.

Akizungumzia hali ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini Dkt. Gwajima amesema jitihada zinazofanyika ili kutokomeza ugonjwa huo zinafanikiwa kwani maambukizo ya malaria yamepungua hadi asilimia 7.3 kutoka asilimia 14.8 kwa mwaka 2015/16.

Amesema kupungua kwa maambukizi ya malaria kumetokana na uwepo kwa mikakati mbalimbali ya kinga na uwepo wa dawa zinazotumika kupambana na ugonjwa huo ambapo kiwango cha matumizi yake kilifikia asilimia 98.4 huku matumizi ya kipimo cha haraka cha kupima vijidudu vya malaria (mRDTs) ikifikia asilimia 97.8.

Gwajima amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la matumizi ya vyandarua vyenye dawa kwa asilimia 62.5 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 55.9 kwa mwaka 2015/16.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa kudhibiti Malaria nchini Dkt. Ali Mohamed amesema kulingana na takwimu za mwaka 2017, mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mara, Lindi, Ruvuma na Mtwara inaoneshla kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria.

Kutokana na takwimu hizi ipo haja ya kuandaa mikakati ya ziada ya kuzuia mbu, kuhakikisha kuna vitendanishi vya kupima malaria na dawa za kutosha zenye ubora unaotakiwa ya jinsi ya kutumia dawa kinga (SP) kwa ajili ya wanafunzi shuleni na maeneo ambayo malaria inapatikana kwa vipindi,” amebainisha Dkt. Mohamed.

Juhudi za kuutokomeza ugonjwa wa malaria Barani Afrika bado zina changamoto kutokana na takwimu za Dunia za malaria za mwaka 2018 kuonesha ripoti za kesi milioni 219 za ugonjwa wa malaria na kusababisha vifo vya watu 435,000 Duniani.

DC Mjema amjibu RC Makonda
Makocha 200 wakitaka kibarua cha Ndayiragije