Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya leo wametia saini makubaliano ya mwisho ya kukamilisha mchakato wa Uingereza kujitoa kutoka umoja huo, Brexit.
Kutiwa saini mkataba huo na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, na Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo, Charles Michel, kutawezesha kuwasilishwa kwake mbele ya Bunge la Ulaya Januari 29 ili kuidhinishwa.
Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wataridhia makubaliano hayo kwa maandishi ifikapo Alhamisi inayokuja kuwezesha Uingereza kutoka ndani ya Umoja huo usiku wa manane wa Januari 31.
Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Baraza Kuu, Charles Michel, amesema licha ya kwamba mambo yatabadilika baada ya Brexit, lakini anajitayarisha kuukaribisha mwanzo mpya wa ushirikiano kati ya Umoja huo na Uingereza.