WAZIRI MAKAMBA; WAKUU WA MIKOA WANA JUKUMU KUBWA MRADI WA EACOP

Waziri wa Nishati, January Yusuf Makamba ameeleza kuwa Wakuu wa Mikoa minane (8) ambapo utapita mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wanajukumu kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuhakikisha fursa zitakazopatikana zinanufaisha wananchi wa mikoa yao husika.

Waziri Makamba ameyasema hayo wakati wa semina kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na mradi huo, inayofanyika jijini Tanga.

“Moja ya sababu za bomba hili kupita nchini kwetu ni uhakika wa ulinzi na usalama uliopo. Usalama huo utaendelea kuwepo kama wanaosimamia usalama huo kwenye maeneo linapopita bomba wana uelewa kuhusu mradi na kile kinachohitajika kufanywa ili walioamua bomba hili lipitie kwetu wawe na imani kwamba walifanya uamuzi sahihi,” Amesema Waziri Makamba.

Ameongeza kuwa semina hiyo inalenga kutengeneza uelewa mpana kwa viongozi hao kuhusu mradi na kujadili fursa mbalimbali zitakazopatikana kwenye utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ametoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ili fursa zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo zinufaishe wananchi wa mikoa husika.

Byabato amesema kuwa Bomba hilo litapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga,Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Ameeleza kuwa Mkataba Hodhi wa Mradi (HGA) baina ya Serikali na Kampuni ya Bomba umeainisha baadhi ya bidhaa na huduma zitakazotolewe na Watanzania pekee (Reserved Contracts).

Naibu Waziri Byabato ameongeza kuwa, bidhaa na huduma hizo ni pamoja na usafirishaji, ulinzi, chakula na vinywaji, huduma ya malazi, mafuta kwa ajili ya magari na mitambo, shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana hapa nchini, shughuli za ujenzi (civil works), huduma za mawasiliano, na ukodishaji wa mitambo ya ujenzi.

Benki ya Dunia kuinua uchumi wa Tanzania
Korea kusini yapiga marufu ulaji wa mbwa