Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa hapa nchini, wametekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako alilolitoa hivi karibuni la kila Mkoa kuwaanda Vijana watakaoshiriki wiki ya Vijana, ambayo kitaifa itaadhimishwa Mkoani Manyara na kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Hayo yamebainishwa hii leo Oktoba 6, 2023 na Katibu Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Injinia Cyprian Luhemeja baada ya kukagua mabanda yaliyoandaliwa katika Viwanja vya Stendi ya zamani yatakapofanyika maadhimisho hayo Kitaifa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Caroline Muthapula amesema maandalizi ya wiki ya Vijana yamekamilika ambapo zaidi ya Vijana 1000 kutoka katika Mikoa mbalimbli ya Tanzania bara na Zanzibar watahudhuria.
Naye, Mratibu wa wiki ya Vijana Mkoa Manyara, Neema Gasabile amesema katika maonesho hayo kutafanyika midahalo mbalimbli, bonanza pamoja na elimu ya ujasiriamali ambayo itawakwamua Vijana kiuchumi katika wiki hiyo ya Vijana itakayoanza Oktoba 8, 2023 na kuhitimishwa Oktoba 13, 2023.