Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi, Vijana na watu wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imetenga jumla Shilingi Bilioni tatu, kwaajili ya ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu na kuviendeleza vyuo hivyo.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo hii leo Juni 29, 2023 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watu wenye ulemavu, iliyoandaliwa Mbunge wa Viti Maalum, Khadija Shaaban Taya (Keisha) na katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Amesema, Serikali pia inaendelea kuweka fursa mbalimbali kwaajili ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwawezesha kufanya ujuzi na bunifu kwa kuwajengea Vyuo vya Ufundi, huku akiwataka kuchangamkia fursa za ajira zinazotangazwa.
Hata hivyo, Prof. Ndalichako amesema mpaka sasa wanajenga vyuo vipya vitatu vya watu wenye ulemavu kwa mikoa mitatu, ikiwemo Kigoma, Songwe na Ruvuma na kuwataka kuchangamkia fursa zinazotolewa kwenye mikopo yao.