Wanufaika wa Mikopo ya Elimu ya Juu wameiomba Serikali kuangalia upya sheria ya makato ya asilimia 15% ya mshahara wanayokatwa na waajiri ili kubaki na kipato cha kutosha kujikimu kimaisha.
Awali, Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB), ilikuwa ikiwakata asilimia 8 wanufaika walioajiriwa lakini mwaka jana Bunge lilipitisha sheria mpya inayomtaka mwajiri amkate mwajiriwa asilimia 15 na wanufaika wasio katika ajira rasmi kukatwa asilimia 10 ya kipato chao.
Hayo yamesemwa na Ofisa Mkuu wa Ubora wa Bidhaa zinazozalishwa na Tanzania Leather Limited, kwa Maofisa wanaoendesha zoezi la msako wa Ofisi kwa Ofisi unaoendeshwa na Bodi hiyo, amesema kuwa kiasi hicho kilianza kutekelezwa Novemba mwaka jana hakijaangalia hali halisi ya mishahara wanayolipwa wanufaika.
“Hebu angalia mtu labda analipwa mshahara wa 400,000, anakatwa kodi, NSSF, bima na hiyo asilimia 15, unabaki na fedha ndogo ambazo ni ngumu kumudu gharama za maisha,”amesema
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji wa Mikopo wa HELSB, Phidelis Joseph, amesema kuwa waajiri watakaobanika kutowasilisha majina ya wanufaika kwa wakati watatozwa faini na kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi 36 jela.