Pichani: Baadhi ya wabunge (sio wote kwenye picha) waliokwenda kumjulia hali Mbowe hospitalini
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alivamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo jijini Dodoma na watu wasiojulikana ambao walimpiga na kumjeruhi.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa Mbowe ambaye anapatiwa matibabu katika Hospitali ya DCMC jijini humo, alijeruhiwa vibaya na watu hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi lakini kwa taarifa za awali, Mbowe ameumizwa kwa kukanyagwa.
“Zipo taarifa kwamba Mheshimiwa Mbowe amevamiwa na watu watatu, amekanyagwa na kuvunjwa mguu wa kulia… lakini tunafuatilia tutatoa taarifa baadaye,” amesema Kamanda Muroto.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema kuwa waliomvamia Mbowe bado hawajajulikana lakini wakati wa tukio walisema maneno yenye muelekeo wa kisiasa.
“Ameshambuliwa jijini Dodoma akiwa anaingia nyumbani kwake, na ameshambuliwa na watu ambao mpaka sasa hivi hawajulikani,” amesema Mnyika.
“Lakini waliokuwa wakimshambulia walikuwa wanazungumza maneno ambayo yanaashiria kwamba walilenga kwenda kumshambulia na shambulizi lake lina muelekeo wa kisiasa. Sasa ni maneno gani, nini hasa kilijili tunaomba mtupe muda sahihi tutawaita vyombo vya habari na tutazungumza,” amesema Mnyika.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, alifika katika hospitali hiyo kumjulia hali Mbowe. Ameeleza kuwa kwa jinsi alivyomuona na kuzungumza naye, Mbunge huyo ameumizwa zaidi katika mguu wake wa kulia.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema kuwa mara ya mwisho alizungumza na Mbowe saa tatu usiku akiwa naye jijini humo.
Imeelezwa kuwa Mbowe atahamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, ingawa bado haijajulikana atahamishiwa katika hospitali gani.
Martin Keown ashauri jambo zito Arsenal
Serikali yaagiza Chuo cha Diplomasia kuongeza tafiti, machapisho