Viongozi wa ngazi za juu wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa pamoja aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na umoja huo, Edward Lowassa jana usiku walikutana na kuteta mjini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar akiungwa mkono na umoja huo pia alihudhuria kikao hicho ambacho taarifa za ndani zimeeleza mambo mawili muhimu waliyojadili.

Imeelezwa kuwa viongozi hao walijadili kuhusu mustakabali wa kisiasa Zanzibar kufuatia kutangazwa kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar Machi 20 mwaka huu kwa mujibu wa tangazo lililotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.

Suala lingine walilojadili ni kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Kamati za Bunge ambao umoja huo uliugomea hivi karibuni  ukidai kuwa umelenga katika kudhoofisha upinzani Bungeni.

“Viongozi wa juu wamejadili mambo mawili, hatma ya Zanzibar na kuhusu Kamati za Bunge zilizoundwa,” chanzo cha ndani kimekaririwa na gazeti la Nipashe.

Uongozi wa CUF umeeleza kuwa utafanya vikao vya juu Januari 27 na 28 mwaka huu kwa lengo la kujadili na kutoa maamuzi waliyofikia kufuatia kutangazwa tarehe ya kurudia uchaguzi huo. Vikao hivyo vitafanyika baada ya kujadili na viongozi wa vyama vingine vya upinzani vinavyounda Ukawa.

 

Mwanasheria Mkuu Mstaafu amshauri Dk. Shein Kujiuzulu
Salim Ahmed Salim ashangaa Tangazo la Kurudiwa Uchaguzi Zanzibar,