Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Morocco Walid Regragui amesema, licha ya kushindwa kutinga Fainali kwenye Michuano ya Kombe la Dunia, kuna jambo kubwa wameionesha Dunia.

Morocco ilishindwa kupenya katika mchezo wa Nusu Fainali jana Jumatano (Desemba 14) baadaya kukubalia kufungwa 2-0 na Mabingwa watetezi Ufaransa.

Kocha Regragui amesema Mashabiki wengi Duniani walikua hawaipi nafasi timu yake, lakini yeye na wasaidizi wake katika Benchi la Ufundi waliamini wanaweza kupambana, na matokeo yake Dunia ilishangazwa na walichokifanya nchini Qatar.

Amesema wanaondoka kwenye Fainali hizo wakiwa na funzo kubwa, ambalo ameahidi watalienzi na kulifanya kazi kwa vitendo, ili watakaporejea tena kwenye Fainali za Kombe la Dunia, waendelee pale walipoishia.

“Wachezaji wangu walitoa taswira nzuri sana ya timu, walionesha ubora wao, walidhamiria kuandika upya vitabu vya historia, lakini tunakubali kushindwa kwa kujifunza, ili tutakaporudi tena tuwe bora zaidi.”

“Unajua Huwezi kushinda Kombe la Dunia kwa miujiza, isipokuwa kwa bidii na ndivyo tutaendelea kufanya, ninaamini hiki kilichotokea hapa kwa kuzifunga timu kubwa Barani Ulaya, kimepeleka ujumbe kwa yoyote kuwa Morocco ni taifa gani, tutarejea tukiwa na nguvu kubwa ziadi naamini ipo siku tutakuwa mabingwa wa Dunia In Shaa Allah.” amesema Kocha Regragui

Morocco wataendelea kusalia nchini Qatar kwa ajili ya kucheza mchezo wa kumsaka Mshindi watatu na wanne, wakitarajia kucheza dhidi ya Croatia Jumamosi (Desemba 17), katika Uwanja wa Khalifa International mjini Al Rayyan.

Mwamuzi Raphael Claus kutoka nchini Brazil amepewa jukumu la kuchezesha mchezo huo, ambao umepangwa kuanza saa kumi na mbili kwa saa za Afrika Mashariki.

Ten Hag aunga mkono Man Utd kupigwa bei
Kibabage anasubiri kutambulishwa Singida BS