WASOMI watatu waliohitimu shahada ya uzamifu (PhD) wamelazimika kufunza shule za chekechea na msingi kwa kukosa kazi katika shule za upili, vyuo vikuu na taasisi husika za serikali.
Dkt John Timon Owenga, Dkt Violet Otieno na Dkt Daughty Akinyi wanasema kwamba wamelazimika kufunza shule za msingi licha ya kubobea katika taaluma zao kwa kuwa hawajafaulu kupata kazi au kupandishwa vyeo.
Dkt Owenga, mwenye umri wa miaka 50 ana digrii ya uzamifu katika Saikolojia ya Elimu, naye Dkt Otieno alihitimu na digrii ya uzamifu katika Elimu ya Chekechea mwaka wa 2018.Wawili hao walisomea chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga.
Mwaka mmoja baadaye, Mwalimu Onyango Daughty Akinyi alihitimu na digrii ya uzamifu baada ya kutia bidii tangu 2003 alipoajiriwa katika kiwango cha P1 kufunza shule za msingi.
Licha ya watatu hao kutumia nguvu, muda, pesa na kujitolea kufikia kiwango cha juu zaidi cha elimu Kenya, hawajaweza kupata kazi zinazolandana na elimu yao katika serikali za kaunti, serikali ya kitaifa, vyuo vikuu au mashirika ya serikali.
Dkt Daughty, anasema kwamba aliajiriwa 2003 na Tume ya Huduma ya walimu (TSC) kufunza katika shule ya msingi ya Anjech, kaunti ya Homa kabla ta kuhamishiwa shule ya msingi ya Atela iliyoko kaunti hiyo.
Mnamo 2013, Daughty alihamia kaunti ya Kisumu anakofunza darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Agai, kaunti ndogo ya Nyakach.
Amekuwa akifunza katika shule za msingi kwa miaka 18 lakini ni miaka mitatu tangu ahitimu uzamifu.
Dkt Owenga ambaye kwa wakati huu ni naibu mwalimu mkuu katika Shule ya Msingi ya Rabuor kaunti ndogo ya Nyando, alisema wanafunzi wake na wazazi wao hushangaa kwa nini anafunza shule ya msingi.
Anasema wakati mwingi kuitwa daktari ni kama laana hasa anapohusiana na wakubwa wake ambao wana viwango vya chini vya elimu kuliko vyao.