Mara baada ya kumaliziki kwa mtihani wa Darasa la Saba siku ya Alhamisi Septemba 12, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, limetoa taarifa ya uwepo wa udanganyifu wa mtihani huo kwa baadhi ya shule mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa polisi Kagera, ACP Revocatus Malimi, amesema kuwa hadi sasa jeshi hilo linawashikilia walimu 10 kwa tuhuma za wizi wa mitihani katika Shule ya Msingi Kumunazi Wilayani Ngara.

Amesema kuwa walimu hao walikutwa wamejifungia kwenye nyumba ya mmoja wa walimu, huku wakiandaa majibu ya somo la Sayansi, tukio ambalo linawajumuisha Walimu wa Shule hiyo pamoja na Walimu wasimamizi, walioteuliwa kusimamia mtihani huo.

”Kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao ni kosa la jinai kwani mitihani ni kipimo cha kuwaandaa na kuwapata wataalamu, licha ya kupewa semina na kula kiapo cha uadilifu ikithibitika wamehusika na udanganyifu wa aina yoyote wakifikishwa mahakamani adhabu yake  ni  kubwa” amesema Kamanda Malimi.

Aidha Malimi amesema, bado wanaendelea na upelelezi na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Mbosso afichua siri yake na marehemu Boss Martha
Polepole amuagiza mkurugenzi kuwatengea mamilioni vijana na wanawake