Wadau wa elimu wilayani Ludewa mkoani Njombe kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali wamedhamiria kuinua kiwango cha taaluma kwa kutoa semina elekezi kwa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu katika kata nne za wilaya hiyo ambayo awali ilikuwa kwenye hali mbaya kielimu.
Kupitia mradi wa MAMIE chini ya shirika la Shipo unaofadhiliwa na shirika la kimataifa la we weld mratibu wa mradi huo bwana Nemes Temba amesema wanatarajia kuona walimu wanaboresha mbinu za ufundishaji kupitia semina hiyo ya siku tisa .
“Katika mkoa wetu wa Njombe tunajua kwenye wilaya sita za mkoa huu wilaya ya ludewa katika taaluma ilikuwa inashika nafasi ya sita au ya tano pale inapojitahidi sana lakini toka tumeanza mradi huu matokeo ya mwaka jana kwa darasa la saba imekuwa ya tatu,kwa hiyo sisi tulipoanza kwenye eneo lile la mradi tu takwimu zilituonyesha ufaulu kwa darasa la saba ulikuwa ni 61% lakini baada ya kutekeleza huu mradi, ufaulu umefikia asilimia 74 kwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mradi”alisema Temba
Baadhi ya walimu wa masomo ya sayansi na hesabu kutoka wilaya ya Ludewa ambao wameanza kupatiwa mafunzo na walimu wabobezi wa masomo hayo toka chuo cha ualimu vikindu cha mkoani pwani, akiwemo mwalimu Godfrey Kimaro na Rahel Nkutile, wamesema semina hiyo itawapa mwanga mpana wa namna ya kufundisha wanafunzi katika shule zao huku wakiiomba serikali kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za wilaya ya ludewa.
Ester Richard ni mkufunzi wa masomo ya sayansi toka chuo cha ualimu Vikindu, amesema jamii haipaswi kuendelea kuogopa masomo ya sayansi kama ambavyo wameaminishwa kwani tanzania ya viwanda haiwezi kufikiwa bila kupata wataalamu wa sayansi.
“Masomo ya sayansi hayana ugumu kama mengine yanahitaji kutia moyo na kuweka bidii kwasabbu yanahitaji vitendo zaidi”aliongeza Ester
Afisa elimu taaluma wilaya ya Ludewa mwalimu Gerion Lugome amewataka walimu hao kwenda kuwaelekeza walimu wenzao kile watakachojifunza kwa siku zote ili kiwe na manufaa katika sekta ya elimu wilayani humo.