Jumla ya Walimu 7,579 ambao ni sawa na asilimia 66.5 kati ya 11,396, wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu kutokana utoro kazini tangu kuanza kwa utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC), mwaka 2016.
Mwenyekiti wa baraza la Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC), Paulina Nkwama ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TSC, na kuongeza kuwa katika kipindi hicho, tume ilitoa uamuzi wa mashauri ya nidhamu 11,396 (asilimia 98.8) kati ya 11,529 yaliyoanzishwa.
Amesema, “Katika makosa yaliyotendwa, kosa la utoro limeongoza kwa kuwa na walimu 7,579 ambayo ni sawa na asilimia 66.5 na makosa mengine tofauti na utoro yakiwa ni asilimia 33.5.”
Nkwama ameyataja makosa mengine kuwa ni pamoja na kughushi vyeti ambayo ni 1,438, mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi 328, ulevi 89 na uzembe kazini yapatayo 56 na kusema tume imetoa uamuzi wa rufaa za Walimu 991 kati ya 1,036 zilizopokelewa na rufaa 45 zipo kwenye hatua ya uchambuzi ili ziwasilishwe mbele ya tume ili kuzihitimisha.