Walimu wilani Sengerema mkoani Mwanza juzi waliandamana hadi katika ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri wakidai kulipwa stahiki zao zilizolimbikizwa.

Wakiwa nje ya ofisi ya Mkurugenzi huyo, walimu hao walieleza madai yao kuwa ni kutopandishwa madaraja ambapo walimu 372 kati yao walipaswa kupandishwa madaraja kwa mujibu wa bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015.

Walimu hao ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Sengerema, Ezekiel Nyamwasa waliongeza kuwa kati yao walimu 972 wilayani humo wameshafikia madaraja husika na wanastahili kupandishwa mishahara lakini hawajapata haki hiyo wakati wengi wao wanakaribia kustaafu. Hivyo, madai yao yasiposhughulikiwa kila mmoja atakuwa amepungukiwa kiinua mgogo cha shilingi milioni 21.

“Ninaidai shilingi milioni 13 za mafunzo, mwaka huu tena ninapandishwa daraja. Nina barua kivuli, silipwi, nina malimbikizo ya mshahara, bado nina matibabu sijapewa, bado nina uhamisho,” alisema mwalimu mmoja.

Hata hivyo, polisi waliingilia kati sakata hilo na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Busenti Bishaija aliwamtaka mwenyekiti wa CWT wilayani humo kuwatangazia wanalimu hao kutawanyika kwani walifanya maandamano kinyume cha sheria.

Baada ya mvutano, walimu hao walikubalina na Mkurugenzi huyo kuchagua wawakilishi 10 watakaowasilisha malalamiko ya walimu hao kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo na kuwapa mrejesho.

Walimu hao walikubali kuondoka katika eneo hilo wakiwaacha wawakilishi wao huku wakiahidi kurudi ofisini hapo kwa maandamano endapo malalamiko yao hayatafanyiwa kazi ipasavyo.

Azam Wafafanua Kuhusu Sakata la Kupotea Makontena Bandarini Yaliyodaiwa Kuwa Ya Bakhresa
Maneno Ya Mtoto Wa Marehemu Mawazo Yaliyowatoa Machozi Waombolezaji, Lowassa Ajitolea Kumsomesha