Halmshauri ya Jiji la Mwanza imewahamisha kwa nguvu kwenye nyumba walizokuwa wanakaa walimu wanne wa shule za sekondari Mlimani, Mapango na Pamba za Jiji hilo, ili kupisha ukarabati unaotekelezwa na Serikali.
Zoezi la kuwaondoa walimu hao kwenye nyumba hizo limefanyika kwa kusimamiwa na askari mgambo baada ya walimu hao kukataa kuhama kwa hiari na kudai hawajalipwa fedha za kufunga mizigo.
Akisimamia zoezi hilo jana kwa niaba Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba, Ofisa Mtendaji wa kata ya pamba, Jonas Mugisha amesema walimu hao wameondolewa kwa nguvu baada ya kukaidi amri ya kuhama kwa hiari kupisha ukarabati wa nyumba hizo.
Amesema walimu hao walipewa barua iliyokuwa ikiwataka kuhama kwenye nyumba hizo ili ziweze kukarabatiwa pamoja na shule hizo kwani serikali imetoa Sh milioni 540.
Mmoja wa walimu hao, Abel Dendwa akizungumza kwa niaba ya walimu hao, amesema ni vema serikali ikaingilia kati suala hilo ili haki iweze kutendeka ikiwamo ya kulipwa fedha zao za kufunga mizigo.