Mkuu wa wilaya ya Igunga John Mwaipopo amewaonya baadhi ya walimu wenye tabia ya ulevi, utoro kazini na wale wanaojihusisha na mapenzi na wanafunzi kuwa siku zao zinahesabika. Kwani tabia hizo zimekuwa na mchango mkubwa sana katika kushusha ufaulu wa wanafunzi shuleni.
Onyo hilo alilitoa juzi alipozungumza na walimu wapatao 380 wakati wa kufungua kikao chao cha kujadili na kuandaa mikakati ya kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuzipongeza shule zilizofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba 2016.
Amesema wapo baadhi ya walimu ambao wamekuwa na tabia ya kujihusisha na vitendo vya mapenzi na wanafunzi, ulevi na hata utoro shuleni huku wakijua kufanya hivyo ni makosa.
Amewaonya Serikali awamu hii ya tano haitavumilia vitendo hivyo vikifanyika watachukulia hatua.
Pia alieleza kuwa Serikali inatambua madai ya walimu na ndiyo maana serikali ya Dk.Magufuli imekuwa ikijitahidi kukusanya mapato ili fedha hizo ziweze kutumika kulipa madeni ya walimu na shughuli nyingine za maendeleo kwa taifa.
Hivyo aliwaomba wawe watulivu wakati madai yao yakishughulikiwa.