Walimu watatu wa Shule ya Sekondari ya Lupoto iliyoko Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wamefariki katika ajali ya gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema kuwa marehemu hao ni David Edwin, Mashaka Mkalafu na Robert Mwakasaka ambao walikuwa miongoni mwa abiria saba ndani ya gari lililopata ajali.
“Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Bwato, kwenye makutano ya barabara ya Matema – Kyela, Jumamosi majira ya saa kumi na moja jioni. Walimu hao walikuwa wanatoka katika hoteli ya kitalii ya Matema Beach, ambako walienda kwa mapumziko ya wikendi,” alisema Kamanda Matei.
“Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliopita kiasi. Lakini pia, dereva wa gari hilo hakuwa na uzoefu katika barabara hiyo ya vumbi ambayo iko kwenye matengenezo,” aliongeza.
-
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 26, 2018
-
Rais wa Zimbabwe azungumzia afya ya Mugabe, ‘hatembei’
Aidha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Mariamu Mgwere alisema kuwa majeruhi wanne wa ajali hiyo wanaendelea na matibabu na kwamba hali zao zinaendelea kuimarika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rungwe, Loema Peter, amesema vifo hivyo ni pigo kwa wilaya hiyo pamoja na Taifa kwa ujumla, kwani walimu watatu walikuwa msaada mkubwa katika vita ya kutokomeza ujinga.
Alisema wawili kati yao walitoka katika Mkoa wa Iringa na mmoja alikuwa mwenyeji wa Wilaya ya Kyela.