Uongozi wa Kampuni ya ulinzi ya Ultimate inayolinda maeneo ya Gymkhana jijini Dar es Salaam, umeeleza jinsi ambavyo askari wake walifanikiwa kumpa msaada Mohammed Dewiji baada ya kutupwa na watekaji, usiku wa manani, Oktoba 20 mwaka huu.
Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Eliuta Mwanjawike amesema kuwa walinzi watatu wa kampuni hiyo waliokuwa zamu ndio waliofanikiwa kukutana na Mo kwa mara ya kwanza baada ya kuachiwa na watesi wake.
Amesema kuwa walinzi wake walimuona mtu anayewafuata akieleza kuwa anahitaji msaada, ndipo walipomwambia asimame alipo na kujieleza.
Mwanjawike aliyefanya mahojiano na Mwananchi amesema kuwa Mo alijitambulisha kwa walinzi hao na kuwaeleza kuwa ndiye aliyekuwa ametekwa na aliwaomba wampeleke katika hoteli ya Holiday Inn ili awapigie simu wazazi wake.
“Askari wangu wakamjibu, Holiday Inn ni mbali, ila ngoja tukuitie usafiri wa ofisi ukupeleke kwenye hoteli hiyo,” Mwananchi wanamkariri Mwanjawike.
“Hata hivyo, Mo aliwaambia hadi gari la ofisi lifike watachelewa hivyo aliwaomba wampeleke kwenye hoteli yoyote iliyo karibu na eneo hilo,” aliongeza.
Alisema walinzi wake wawili kati ya watatu waliokuwepo walimpeleka katika hoteli ya Southern Sun, iliyoko karibu zaidi na eneo (takribani mita 210) hilo kwa kulinganisha na ilipo Holiday Inn.
Alisema kuwa walinzi hao walisubiri hadi ndugu wa Mo Dewji walipofika na kumchukua katika hoteli hiyo, ndipo walipoondoka kurejea katika kituo chao cha kazi.
Kwa mujibu wa Msemaji wa familia ya bilionea huyo, Azziz Dewji baada ya kumfuata katika eneo hilo walimpeleka moja kwa moja nyumbani.
“Afya yake ni kamilifu kwa asilimia 100, labda tu saikolojia yake kidogo kutokana na tukio la kutekwa,” alisema Azziz.
Mo alitekwa Oktoba 11 katika hoteli ya Colosseum iliyoko Osterbay jijini Dar es Salaam, alipokwenda kufanya mazoezi majira ya saa 11 alifajiri.