Idadi rasmi ya waliokufa kutokana na mafuriko tangu msimu wa mvua nchini Sudan kuanzia mwezi Mei hadi Septemba, 2022 imefikia watu 134, ambapo kwa wiki lililopita pekee watu 20 walifariki kutokana na matukio mbalimbali yaliyosababishwa na mvua.
Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Ulinzi wa Raia la Sudan, Brig. Jenerali Abdul-Jalil Abdul-Rahim amesema watu zaidi ya 120 walijeruhiwa kutokana na mafuriko ya wiki iliyopita, na kwamba mvua zimeharibu barabara, nyumba na miundombinu muhimu nchini kote.
Amesema, pia mvua hizo zimekata njia za usambazaji wa huduma ikiwemo kukatwa kwa umeme kwa maeneo ya vijijini ambayo mengi yameharibiwa vibaya na yanahitaji msaada wa kibinadamu ili kunusuru hali za majeruhi na watu waliokosa chakula na matibabu.
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu mafuriko, takriban watu 286,400 wameathiriwa na mafuriko na nyumba 16,900 zimeharibiwa na aeneo ya mashambani yaliyopo mashariki na magharibi mwa nchi ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na mvua za mwaka huu.
Mapema hivi karibuni, Baraza hilo la ulinzi wa raia lilisema, vifo vya mwaka huu ni pamoja na watu 74 waliokufa maji, 32 waliokufa wakati nyumba zao zilipoporomoka, na sita waliokufa kutokana na kupigwa na shoti ya umeme baada ya maji kujaa.
Septemba 14, 2022, chombo cha Habari cha Serikali ya Sudan (SUNA), kiliripoti kuharibika kwa kiwanda kipya cha sukari kilichojengwa karibu na mji wa Kassala kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, na ikumbukwe kwamba mwaka wa 2020, mafuriko na mvua kubwa ziliuwa karibu watu 100 na kuharibu zaidi ya nyumba 100,000.